Saturday, October 11, 2008

Basaleh: Haya ndiyo yaliotaka kumpigisha Gorogosi

MHADHIRI maarufu wa dini ya kiislam wa msiki wa kwa Idriis jijini Dar es Salaam, Sheikh Ali Basalehe amesema chanzo cha vurugu zilizotokea katika uzinduzi wa Mtaala mpya wa elimu ya Dini ya kiislaam kwa shule za msingi Jumaamosi katika ukumbi wa Jeffery (zamani Korea) iliyopita inatokana na Wislaam kuona kuwa wanadharauliwa.

Alisema dhana hiyo imekuja kutokana na uwamuzi wa Jumuiya ya Walimu wanaosomesha Kur-an Tanzania Bara (JUWAKUTA) kuishirikisha Taasisi ya Konrad Adamuer Stiftung ya Ujerumani ambayo ni ya Kikristo badala ya kuwashirikisha Waislaam wenyewe.

Sheikh Baselehe aliyasema hayo jana mara baada ya sala ya Ijumaa iliyosaliwa katika msikiti huo Kariakoo jijini Dar es Salaam.

Sheikh Baselehe alisema uislaamu unapenda umoja na kushauriana juu ya mambo yote yanayowahusu waislaamu na kuongeza kuwa hayo ndiyo yaliyomfanya Mtume Muhammada (S.A.W) kufanikiwa sana katika uongozi wake.

Alisema kama utaona kiongozi au Taasisi inapingwa na watu wake ni kutokana na jeuri na kiburi cha viongozi au Taasisi hiyo.

Alifafanuwa kwamba kama Juwakuta ilikuwa na nia nzuri basi ingeliwashirikisha Waislaam nchini kwa sababu ndio wadau wakubwa wa Mtaala huo wa umoja.

Alisema pia Juwakuta haikubainisha matatizo ya Mtaala uliopo wa dini ya kiislaam ambao unatumika kuanzia shule za msingi hadi sekondaeri.

Alihoji kuwa kwa vile wapo walioandaa mtaala unaotumika hivi sasa kwa nini Juwakuta haikuwashirikisha badala yake inashirikiana na Taasisi ya kikristo ambayo asili yake ni jina la kiongozi mmoja wa zamani wa Ujerumani.

Alisema Taasisi hiyo ni kitengongo cha chama cha siasa cha Christian Democratic Union (CDU) cha Ujerumani ambacho lengo lake ni kukuza na kuendeleza imani ya dini ya kikristo.

Alisema akiwa katika moja vikao vya kielimu na Taasisi ya elimu ya serikali, mtu mmoja ambaye alikuwa mkristo alihoji kwa nini Waislaam wanaboresha mtaala wa dini yao wakati wao hata mtaala wa somo la Bibilia hawana.

Sheik Baselehe alihoji pia kwa nini Taasisi hiyo ya Konrad haikushirikiana na Wakristo na kuandaa mtaala wa somo la Bibilia ambalo halina mtaala na badala yake inashirikiana na Waislaamu.

“Hivi ni nani anapaswa kusaidiwa kati ya mwenye nacho na asiekuwa nacho au kati ya aliyeshiba na mwenye njaa” alihoji Sheik Básale.

Básale alisema kuwa jitihada za kuwabadilishia Waislaam mifumo yao ya mafunzo ya dini hazikuanza leo na ni mkakati maalumu unaofadhiliwa na Marekani ambao kwa dhana zao potofu ndio inasababisha ugaidi na kutoa mfano wa dini mseto na kupingwa kwake vikali na Waislaam.

No comments: